RWANDA

Watu sita wapoteza maisha baada ya jengo kuporomoka nchini Rwanda

Watu sita wamepoteza maisha na zaidi ya thelathini wamejeruhiwa baada ya jengo kuporomoka Kaskazini Mashariki mwa Rwanda huku zoezi la uokozi likitamatishwa hii leo siku moja baada ya tukio hilo.

naharnet.com
Matangazo ya kibiashara

Polisi nchini humo wamesema kuwa watu sita waliokuwa wakifanya kazi katika jengo hilo wamefariki dunia kutokana na kuangukiwa na jengo hilo na kuongeza kuwa wote waliopteza maisha na waliojeruhiwa walikuwa wakifanya kazi katika jengo hilo ambalo sehemu yake ilikuwa imemalizika.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa watu wapatao 100 wanahofiwa kunasa kwenye kifusi cha jengo hilo lakini kadiri zoezi la uokozi lilivyoendelea idadi hiyo ilipungua ambapo watu thelathini waliokolewa wakiwa hai.

Mkuu wa polisi Eric Mutsinzi amethibitisha kukamilika kwa zoezi la uokozi na kuongeza kuwa watu watatu kati ya majeruhi 30 wamepelekwa katika hospitali ya Kigali wakati wengine 15 wamesalia katika hospitali ya mji wa Nyagatare.