KENYA

Makabiliano ya kikabila Kaskazini mwa Kenya yahofiwa kusababisha vifo vya watu 20

Watu 20 wanahofiwa kuuawa katika mji wa Moyale Kaskazini Mashariki mwa Kenya kutokana na makabiliano ya kikabila yanayoendelea.

Matangazo ya kibiashara

Gavana wa jimbo la Marsabit, Ukur Yattani akizungumza na Gazeti la kila la Daily Nation amesema kuwa watu 20 wamepoteza maisha siku ya Jumatano na makabiliano hayo yanaendelea.

Maafisa wa usalama na wa kisiasa wamekuwa wakikutana katika kikao cha dharura kujadili suluhu ya machafuko hayo ambao yalianza mapema juma hili.

Awali, serikali ilitangaza kuwa ni watu sita ndio waliokuwa wameuawa na tayari jeshi la kupambana na ghasia limetumwa katika eneo hilo kulinda amani.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo Gatiria Mboroki amesema kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini walioanzisha mapigano  hayo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Polisi wanasema kuwa makabiliano hayo yalianza baada ya kundi la watu wa jamii ya Gabra kumshambulia Mborana kwa kumpiga risasi .

Makabila ya Borana na Gabra kwa kipindi kirefu yamekuwa yakishuhudiwa Kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na kugombania maeneo ya kulisha mifugo.