KENYA

Kenya yakanusha madai ya kuyashawishi mataifa ya Afrika kujiondoa ICC

Serikali ya Kenya imekanusha kuwa na mpango wa kuzishawishi nchi zingine barani Afrika kujiondoa katika mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya Kimataifa ya ICC.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Balozi Amina Mohammed amesema kuwa kinachoshuhudiwa barani Afrika ni ungwaji mkono kutoka kwa mataifa ya Afrika yanayotaka kusitishwa kwa kesi zinazowakabili viongozi wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC.

Aidha, Waziri huyo amekanusha kuwa mkutano wa dharura wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mwishoni mwa juma hili Jijini Addis Ababa Ethiopia umeitishwa mahsusi kujadili kuhusu kesi za ICC zinaendelea mjini Hague.

Kauli ya Mohammed inakuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma kuwauliza wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa watakavyojibu ikiwa wataombwa kuhusu kesi hizo kurudishwa nchini Kenya.

Kesi ya rais Kenyatta inatarajiwa kuanza mwezi ujao anakotuhumiwa kuchochea na kufadhili machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka 2007 na kusababisha zaidi ya watu 1000 kupoteza maisha yao.

Mawakili wa Kenyatta wanasubiri uamuzi wa Mahakama hiyo baada ya kuwasilisha ombi la kumtaka Kenyatta kuhuduria vikao hivyo kupitia mtandao wa Video.

Kenyatta atakuwa rais wa kwanza katika historia ya Mahakama hiyo kushstakiwa akiwa uongozini.

Kesi ya naibu wake inaendelea mjini Hague.