TANZANIA-ZANZIBAR-Muziki

Tamasha la Muziki la “Sauti za Busara” Februari 13–16 mjini Zanzibar

Tamasha la muziki, Zanzibar februari 13-16 mwaka 2014
Tamasha la muziki, Zanzibar februari 13-16 mwaka 2014

Tamasha la Muziki la Zanzibar maarufu kama Sauti za Busara ni tamasha amabalo hufanyika barani Afrika kila mwaka mwezi Februari katika mji mkongwe wa Zanzibar nchini Tanzania. Ni tamasha ambalo huwajumuisha wasanii kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na nje ya bara hilo. “ Lengo ni kuwaleta pamoja watu na kuonyesha utajiri wa muziki wa kisasa ambao umebuniwa katika nchi za Afrika mashariki, nchi nyingine kutoka barani Afrika na kwingineko duniani.”

Matangazo ya kibiashara

Makala ya 11 ya tamasha hilo yatafanyika mwaka huu kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 Februari katika viwanja vya kihistoria vya Ngome Kongwe, zanzibar. Tamasha hili litaanza rasmi tarehe 13 Februari majira ya saa kumi na moja jioni kwa muziki wa Taarab utakaotumbwizwa na kikundi cha muziki cha Baladna Taarab cha Zanzibar.

Mbali na maonyesho ya papo kwa papo ya muziki, tamasha la Sauti za Busara linajishughulisha pia na mambo mengine yakiwemo mitindo, na maonyesho mbalimbali yanayohusiana na tamasha hilo kama maonyesho ya matembezi katika mitaa ya mji.

Miongoni mwa wasanii maarufu wanaotarajiwa kuwasili na kushiriki katika tamasha hilo ni pamoja na Jupiter & Okwess International wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Noumoucounda Cissoko kutoka Senegal, Tritonik wa Visiwa vya Mauritius na wengine wengi.

Kwa Mujibu wa Afisa Habari wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, kati ya zaidi ya maombi 500 yaliyowasilishwa, vikundi takriban thelathini tu ndivyo vilivyochaguliwa kushiriki katika Tamasha hilo na kushirikisha Wasanii wapatao 200.

Kauli mbiu ya mwaka huu, kama ilivyo ada, ni “Asilimia mia moja, Muziki wa kiafrika Live”.

Aidha mafunzo yatatolewa katika muktadha wa tamasha hilo ikiwemo pamoja na warsha za mafunzo “ kuwajenga uwezo na ujuzi wasanii, mameneja, wanahabari wa muziki, watengeneza filamu, mafundi wa sauti na mafundi wa taa kutoka eneo la Afrika mashariki”.

Hili ni tamasha ambalo pia lina sifa ya kuwavutia watalii wengi na kukuza sekta hiyo nchini Tanzania na kutoa fursa za ajira kwa wazawa wa Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla. Kwa “muda wote wa tamasha, kisiwa cha Zanzibar kinarindima kwa matukio ya kufurahisha: ngoma za kiasili na wachezaji, maonyesho ya mitindo, mbio za ngalawa, vikao vya wazi, burudani pamoja na muziki wa taarab wenye asili za Zanzibar. Vyote hivi vinaandaliwa na wenyeji wa Zanzibar”, bila kusahau filamu za aina tofauti.

Kwa habari na maelezo zaidi tembelea tovuti ya Sauti za Busara http://www.busaramusic.org