Kanisa Katoliki lawatambua mashoga
Imechapishwa: Imehaririwa:
Maaskofu wa Kanisa Katoliki duniani wamekutana katika makao makuu ya Kanisa hilo mjini Vatican na kuafikiana kuwatambua watu wanaojihusisha na ndoa ya jinsia moja.
Maaskofu hao wamesema, watu hao wana vipaji wanavyoweza kutumia kulisaidia Kanisa na hivyo hawawezi kutengwa na Kanisa hilo.
Hata hivyo, Maaskofu hao hawajesema kuwa wanaounga mkono ndoa za jinsia moja, lakini Mashirika yanayotetea haki za mashoga na wasagaji wanasema hatua ya kutambuliwa na Kanisa Katoliki ni ya kutia moyo.
Mbali na suala hilo, Maaskofu hao zaidi ya 200 ambao wamekuwa wakikutana tangu tarehe 5 mwezi huu wamekuwa pia wakijadili utoaji mimba, dawa za kuzuia mimba na talaka.
Zaidi ya maaskofu 200 wa kanisa katoliki wanakutana kwenye mkutano wa Synodi tangu mapema mwezi huu, katika mkutano huo ni papa Francis aliyetoa mwito wa kujadili masuala ya utoaji wa mimba, vidonge vya uzazi wa mpango,mapenzi ya jinsia moja na talaka.
Papa Francis amewataka viongozi wa juu wa kanisa hilo kuzingatia zaidi suala la wapenzi wa jinsia moja kuliko kuwatenga .
Kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki anazichukulia ndoa hizo za jinsia moja kama zisizo na utaratibu akiinukuu ripoti ya kanisa katoliki iliyochapishwa mwaka 1986, wakati alipokua mshauri mkuu wa Papa John Paul, anaye husika na masuala ya teolojia ya Kanisa Katoliki .