BURUNDI-JAMII

Rais wa zamani wa Burundi afariki

Ilikuwa Machi 28, 2000 mjini Arusha: Nelson Mandela, mpatanishi katika mazungumzo ya amani Burundi (wa 2 kutoka kushoto) katikati ya Rais Pierre Buyoya (kushoto), Jean-Baptiste Bagaza (wa 2 kutoka kulia) na Silvestre Ntibantungana (kulia).
Ilikuwa Machi 28, 2000 mjini Arusha: Nelson Mandela, mpatanishi katika mazungumzo ya amani Burundi (wa 2 kutoka kushoto) katikati ya Rais Pierre Buyoya (kushoto), Jean-Baptiste Bagaza (wa 2 kutoka kulia) na Silvestre Ntibantungana (kulia). ALEXANDER JOE / AFP

Rais wa zamani wa Burundi Jean-Baptiste Bagaza amefariki Jumatano, Mei 4 nchini Ubelgiji, ambapo alikuwa amelazwa hospitalini, baada ya afya yake kuwa matatani kwa muda mrefu.

Matangazo ya kibiashara

Rais Bagaza alichukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1976, baada ya kuung'oa utawala wa mtangulizi wake Michel Micombero, aliyeuangusha utawala wa kifalme mwaka 1966.

Rais Jean-Baptiste Bagaza aliongoza nchi ya Burundi kwa kipindi cha miaka 11 (1976-1987). Hata hivyo rais Bagaza, kutoka jamii ya watu walio wachache nchini humo (Watutsi) alipinduliwa madarakani mwaka 1987 na Pierre Buyoyo, mwanajeshi wa cheo cha Meja kutoka vile vile jamii ya Watutsi.

Katika kipindi chote hicho cha utawala wake, Rais Bagaza alijihusisha na maendeleo katika sekta mbalimbali: umeme, elimu, miundombinu, maji safi, ujenzi wa miji ... Na amani na utulivu vilishuhudiwa katika kipindi chote hicho.

Baada ya kipindi kirefu kukishuhudiwa hali ya sintofahamu nchini Burundi toka wakati Michel Micombero alipochukulia hatamu ya uongozi wa nchini mwaka 1966, na kufuatiwa mauaji ya watu kutoka kabila la Watutsi, na baadaye jamii hii ya wwatuttsi kujilipiza kisase kwa kuwaangamiza viongozi, matajiri na watu maarufu kutoka jamii ya wahutu mwaka 1972, mauaji ambayo yalitajwa kuwa ya kimbari.

Kufuatia kifo hicho cha rais Jean-Baptiste Bagaza, serikali ya Burundi imetangaza maombolezo ya kitaifa ya siku tatu.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoendeshwa na jeshi chini ya uongozi wa Meja Pierre Buyoyo, Kanali Jean-Baptiste Bagaza alijaribu kuingia nchini Burundi bila mafanikio. Aliishi ugenini kwa zaidi ya miaka mitano. Alirudi nchini baada ya rais Melchior Ndadaye kuchukua hatamu ya uongozi wa nchi kufuatia ushindi wa chama chake cha FRODEBU. Rais Melchior Ndadaye alikua rais wa kwanza kutoka jamii ya Wahutu aliyechaguliwa kupitia mfumo wa vyama vingi.

Marais wote watatu waliopinduana kijeshi ni kutoka kabila moja na kijiji kimoja, katika mkoa wa Bururi, kusini mwa Burundi.

Rais Bagaza, 69, Seneta wa kudumu, hakuwahi kujiondoa katika siasa, licha ya afya yake kuwa matatani katika miaka ya hivi karibuni.