KENYA-SIASA

IEBC yapinga kata kata kujiuzulu

Mji mkuu wa Kenya Nairobi.
Mji mkuu wa Kenya Nairobi. Reuters/Noor Khamis/File Photo

Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC inasema haijiuzulu licha ya kuendelea kupata shinikizo kutoka kwa wanasiasa wa upinzani kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe wa Tume hiyo wanasema, wao sio mafisadi na wala hawaegemei upande mmoja kama inavyodaiwa na muungano wa CORD.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Isaak Hassan akizungumza leo na wanahabari jijini Nairobi amesema, wako tayari kukutana na wadau wote kujadili maswala yanayolalamikiwa na wao hawawezi kujiuzulu kwa sababu hawana kosa na wanaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa mwakani.

Wanasiasa wa upinzani wanatishia kutoshiriki katika uchaguzi wa mwakani ikiwa tume hiyo haitafanyiwa marekebisho na Jumatano wiki hii walizundua vuguvugu linalofahamika kwa jina la Firimbi Movement kupiga kambi kila Jumanne katika Makao Makuu ya Tume hiyo kuendelea kushinikiza kujizulu kwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi.

Wakati hayo yakijiri, baada ya siku sita kufunikwa na vifusi vya jengo la makazi ya ghorofa saba lililoporomoka katika mtaa wa Huruma jijini Nairobi nchini Kenya, watu wanne ikiwa ni pamoja na mwanamke mja mzito wametolewa chini ya vifusi wakiwa hai.

Maafisa wa uokoaji wanasema watu hao wamepelekwa hospitalini na wanaendelea kupata matibabu. Inaarifiwa kuwa mwanamke huyo mja mzito hakupata jeraha lolote mwilini.

Mapema wiki hii, mtoto wa mwaka mmoja pia alitolewa chini ya vifusi akiwa hai.

Hata hivyo, idadi ya watu waliopoteza maisha imefikia sasa 36.