Vyombo vya habari Uganda vyachukuliwa hatua
Imechapishwa:
Serikali ya Uganda imepiga marufuku vyombo vya habari nchini humo kupeperusha matangazo ya moja kwa moja kuhusu maandamano ya upinzani yakiongozwa na Kizza Besigye kutoka chama cha FDC kuendelea kupinga ushindi wa rais Museveni mwezi Februari.
Hii inamaanisha kuwa vyombo vya Habari haviruhusiwi kuwahoji wanasiasa wa upinzani au kuonesha shughuli zao za kisiasa wakati huu rais Museveni akitarajiwa kuapishwa Alhamisi ijayo.
Besigye ameendelea kudai kuwa alishinda uchaguzi uliopita, ametangaza kuongoza maandamano dhidi ya rais Museveni lakini pia kusema ataapishwa sambamba na rais Museveni, shughuli ambazo zimezuiwa na Mahakama.
Waziri wa Habari wa Uganda Jenerali Jim Muhwezi amesema vyombo vya habari vitakavyokwenda kinyume na marufuku haya, vitachukuliwa hatua kali za kisheria
Hayo yakijiri polisi nchini nchini humo wametumia mabomu ya kutoa machozi kusambaratisha maandamano ya wafuasi wa upinzani dhidi ya rais Yoweri Museveni jijini Kampala, huku baadhi ya waandamanaji wakikamatwa.