KENYA-CORD-SIASA

Upinzani waandamana mbele ya Ofisi ya IEBC Kenya

Raila Odinga, Waziri Mkuu wa Kenya, na Kiongozi mkuu wa upinzaniJulai 7, 2014 Nairobi.
Raila Odinga, Waziri Mkuu wa Kenya, na Kiongozi mkuu wa upinzaniJulai 7, 2014 Nairobi. REUTERS/Noor Khamis

Muungano wa upinzani nchini Kenya CORD umekuwa na maandamano ya amani mbele ya Ofisi ya Tume ya Uchaguzi IEBC jijini Nairobi, kuendelea na shinikizo za kuwataka Wajumbe wa tume hiyo kujizuulu kwa madai kuwa hawako huru kusimamia Uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Kuanzia Jumatatu hii asubuhi wafuasi wa muungano huo unaoongozwa na Raila Odinga ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu, walianza kuwasilia nje ya Ofisi ya Tume ya Uchaguzi, eneo ambalo lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wa kupambana na ghasia.

Maandamano ya leo yalikuwa ya pili, baada ya mengine kufanyika wiki mbili zilizopita, na kuishia katika makabiliano kati ya wafuasi wa upinzani na polisi.

Kabla ya kuwasili kwa viongozi wa CORD, Mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi, Japhet Koome, alisema polisi walikuwa wamejiandaa kupambana na waandamanaji ikiwa kutakua fujo.

Hata hivyo, waandamanajii waliokuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kuwataka Wajumbe hao kujiuzulu, walionekana wakiimba na wengine wakipuliza firimbi kuwasubiri viongozi wao.

Viongozi wakuu wa Upinzani wakiongozwa na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula waliwasili baadaye mchana na kuanza kuwahutubua wafusi wao.

Musyoka ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa rais amesema tume hiyo ya uchaguzi inapanga kuiba kura kwa kuwasajiki watoto kama wapiga kura.

Madai hayo yalisisitizwa na Bwana Odinga ambaye alisema muungano huo utaendelea kushinikiza Wajumbe hao kujiuzulu.

Aidha, amesisitiza kuwa maandamano hayo yataendelea katika Ofisi ya Tume hiyo hadi pale watakapojizulu.

Madai ya upinzani yamekanushwa na Tume hiyo inayoongozowa na Isaak Hassan ambaye wiki iliyopita alisema hatajizulu kuelekea Uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Hata hivyo polisi imetumia mabomu ya machozi kwa kuwatawanya waandamanaji.