Yoweri Museveni kutawazwa Alhamisi
Imechapishwa: Imehaririwa:
Rais wa Uganda Yoweri Museveni anaapishwa leo Alhamisi katika uwanja wa Kololo kuongoza tena nchi hiyo kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Museveni mwenye umri wa miaka 71 na ambaye ameongoza nchi hiyo kwa miaka 30 sasa alitangazwa mshindi baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi Februari.
Usalama umeimarishwa jijini Kampala huku wanasiasa wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama cha FDC Kizza Besigye wakizuiliwa nyumbani kwao.
Chama cha FDC ambacho kinadai kilishinda uchaguzi huo, nacho kilitangaza kumwapisha kiongozi wao.
Serikali imesema imewaalika wagombea wote waliowania urais kushiriki katika sherehe za kumwapisha rais Museveni kesho ambazo pia zitahudhiriwa na viongozi wengine wa Afrika.
Hata hivyo chama cha upinzani cha FDC nacho kimesema kimemwalika rais Museveni kuja kushuhudia kuapishwa kwa Kizza Besigye.
Mitandao ya kijamii ilifungwa jana Jumatano baada ya kusamba kwa video ya kiongozi wa upinzani Kizza Besigye akiapishwa.