SWEDEN-RWANDA-MAUAJI

Claver Berinkindi ahukumiwa kifungo cha maisha jela Sweden

Mahakama moja nchini Sweden imemuhukumu raia wa Sweden mwenye asili ya Rwanda kifungo cha maisha jela kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama imetoa uamuzi kuwa Claver Berinkindi, mwenye umri wa miaka 61, kutoka jamii ya Wahutu, amepatikana na hatia ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kupita kiasi kama vile mauaji, jaribio la mauaji na utekaji nyara chini ya sheria za kimataifa.

"Hii inahusiana na ushiriki katika idadi kubwa ya mauaji wakati wa mwaka 1994 ambapo mtuhumiwa alikua kiongozi wa kundi la lililokua likiendesha mauaji hayo," hukumu ya mahakama imebainisha.

Sheria ya Sweden inaruhusu Mamlaka ya kisheria kuchukua uamuzi kwa raia sweden au raia wa kigeni kwa uhalifu uliofanywa nje ya nchi hiyo.

Zaidi ya watu 800,000, wengi wao kutoka jamii ya watu wachache ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani, waliuawa na Wahutu mwaka 1994 kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hii ni mara ya pili Mahakama yaSweden inatoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya kimbari yaliyotokea nhini Rwanda. Hukumu ya kwanza ilitolewa mwaka 2013.