BURUNDI-RWANDA-WAKIMBIZI

Rwanda yawafukuza Warundi 1,500

LWakimbizi wa Burundi walio uhamishoni katika nchi jirani ya Tanzania
LWakimbizi wa Burundi walio uhamishoni katika nchi jirani ya Tanzania (Carine Frenck)

Rwanda iliwafukuza siku za hivi karibuni mamia ya raia wa Burundi waliokua katika ardhi yake. kwa mujibu wa serikali ya Rwanda, raia hao walikuwa hawatimizi masharti ya kuishi Rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa maswala ya Majanga na wakimbizi wa Rwanda Seraphine Mukantabana amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika kuwa raia hao walikuwa wanaishi nchini humo bila ya kuwa na vibali vinavyohitajika.

Kwa mujibu wa Seraphine Mukantabana, Waziri wa Rwanda mwenye dhamana ya Wakimbizi, zoezi hili la kuwafukuza raia hao lilifanyika kama sehemu ya operesheni ya kawaida kwa raia wa kigeni wanaoishi nchini Rwanda kinyume cha sheria.

"Tulikuwa na idadi ya raia wa Burundi waliokua wametawanyika nchini kote na ambao hawakuwa na vibali vinavyowaruhusi kuishi nchini hapa," Waziri Mukantabana amesema. "Tuliwaomba kutafuta vibali au kutafuta hadhi ya ukimbizi lakini walipuuzia. Wale waliokataa kutekeleza masharti hayo walirejeshwa nyumbani kwao, " amendelea kusema, huku akihakikisha kuwa hajui idadi kamili ya watu waliorejeshwa Burundi.

Haya yanajiri wakati huu, uhusiano kati ya nchi hizi mbili ukiendelea kuyumba kutokana na madai ya Burundi kuwa Rwanda inawapa mafunzo ya kijeshi wakimbizi waliokimbilia nchini humo ili kumwondoa madarakani rais Piere Nkurunziza.

Mwaka uliopita, Burundi nayo iliwafukuza maelfu ya raia wa Rwanda waliokuwa wanaishi nchini humo kinyume cha sheria.