KENYA

Maandamano ya upinzani yaanza nchini Kenya

Maandamano ya wiki zilizopita
Maandamano ya wiki zilizopita REUTERS

Maandamano ya upinzani yanaendelea katika miji mbalimbali nchini Kenya kushinikiza kujiuzulu kwa Makamishena wa tume ya uchaguzi IEBC kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Jijini Nairobi, waandamanaji wanakutana katika bustani ya Uhuru kuelekea katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi katika Jumba la Anniversary Towers.

Mjini Kisumu na Migori Magharibi mwa nchi hiyo, shughuli zimekwama huku barabara kuu ya kuelekea Kakamega ikifungwa na matairi ya magari kuteketezwa moto.

Wakati uo huo, Mahakama kuu jijini Nairobi imekubali kufanyika kwa hayo na kutaka polisi kutoa usalama kwa waandamanaji, baada ya mbunge wa serikali kutaka maandamano hayo kuzuiliwa.

Hata hivyo, Kamanda wa jeshi la polisi jijini Nairobi Japhet Koome ameonya kuwa nguvu kupita kiasi itatumiwa kuwasambaratisha waandamanaji na hata kuwakamata viongozi wa upinzani akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.