KENYA

Watu wawili wauawa katika maandamano ya upinzani nchini Kenya

Maandamano ya upinzani nchini Kenya
Maandamano ya upinzani nchini Kenya REUTERS/Goran Tomasevic

Watu wawili wameuawa na wengine kujeruhiwa katika maandamano ya upinzani mjini Kisumu nchini Kenya, kushinikiza kujiuzulu kwa Makamishena wa tume ya uchaguzi siku ya Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema watu hao walipigwa risasi na maafisa wa polisi baada ya kuzuka kwa makabiliano kati ya walinda usalama na waandamanaji.

Inaelezwa kuwa waandamanaji walifunga barabara kuu ya kwenda mjini Kakamega na kuwasha moto matairi ya magari pamoja na kulipiga kwa mawe duka moja la jumla.

Machafuko kama hayo pia yaliripotiwa mjini Migori ngome nyingine ya CORD Magharibi mwa nchi hiyo.

Waandamanaji mjini Kisumu
Waandamanaji mjini Kisumu REUTERS

Jijini, Nairobi maandamano yalikuwa ya amani na kuongozwa na vinara wa CORD Raila Odinga na Moses Wetangula baada ya Mahakama kuamuru kuwa upinzani una haki ya kuwa na maandamano ya amani kwa mujibu wa Katiba.

Aidha, Odinga amesisitiza kuwa maandamano haya yataendelea hadi pale serikali itakapokubali mazungumzo au Makamishena watakapojiuzulu.

Upinzani unasema kuwa wiki ijayo, maandamano hayo yatafanyika siku ya Jumatatu na Alhamisi na baadaye kila siku ikiwa mwafaka hautapatikana baada ya wiki mbili kutoka sasa.

Waandamanaji mjini Migori
Waandamanaji mjini Migori Daily Nation

Serikali inasema iko tayari kwa mazungumzo lakini kupitia bunge lakini upinzani unataka mazungumzo hayo yafanyike nje ya bunge.

Kenya inatarajiwa kuwa na uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Maandamano ya upinzani Kenya
REUTERS/Thomas Mukoya