KENYA-SOMALIA

Mpango wa Serikali ya Kenya waendelea kukosolewa

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab, kaskazini mwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya Aprili 28, 2015.
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab, kaskazini mwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya Aprili 28, 2015. AFP PHOTO/Tony KARUMBA

Tume ya haki za binadamu nchini Kenya, inasema kuwa mpango wa Serikali kutaka kuifunga kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Daadab, inakikuka sheria za kimataifa na inaenda kinyume na katiba.

Matangazo ya kibiashara

Tume hiyo inaitaka mahakama kuu nchini humo kuingilia kati suala hilo, kwa kusikiliza haraka shauri lao waliloliwasilisha mahakamani kupinga mpango wa Serikali wa kuifunga kambi hiyo inayowahifadhi zaidi ya wakimbizi wa Somalia laki 3 na elfu 50.

Hatua hii ya tume ya haki za binadamu nchini Kenya inakuja ikiwa ni siku moja tu imepita toka rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud atembelee kambi ya Daadab ambako alikutana na raia waliokimbia nchi yake kutokana na hali mbaya ya usalama.

Rais Sheikh Mohamoud juma hili anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake rais Uhuru Kenyatta kwenye Ikulu ya Nairobi, mkutano unaoelezwa kuwa watazungumzia suala la kuifunga kambi hiyo.

Rais Kenyatta kwa upande wake anasisitiza kuwa mwezi November mwaka huu kambi hiyo lazima ifungwe, na kwamba Serikali yake inaandaa utaratibu mzuri ambao utawafanya wakimbizi hao wasijisikie kama wanafukuzwa kwa nguvu kurudi nyumbani.

Mpango huu wa Kenya kutaka kuifunga kambi ya Daadab ifikapo mwezi November mwaka huu, unakosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa.

Hayo yakijiri Serikali ya Kenya imetangaza kutenga kiasi cha shilingi milioni 500 ikiwa ni sehemu ya kuendesha kampeni yake ya kuhamasisha utalii kutoka nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki, jitihada zinazolenga kukabiliana na kushuka kwa kiwango cha watalii wanaotembelea nchi hiyo kutoka nchi wanachama.

Waziri wa utalii nchini Kenya, Najib Balala, amesema kuwa kampeni ya mwaka huu inalenga kuwavutia watalii kutoka nchi za Tanzania, Uganda na Rwanda, ambapo idadi ya watalii kutoka kwenye nchi hizi imeshuka kwa kiwango kikubwa.

Balala amesema kuwa nchi yake imepoteza kiasi cha shilingi bilioni 12 kutokana na kupungua kwa watalii, huku akionya mvutano wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa kwa sasa unatishia zaidi kuikosesha mapato nchi kupitia utalii.

Kampeni kama hii ilifanikiwa kwa kiwango kikibwa mwaka jana ambapo Serikali ilifanikiwa kuwashawishi watalii kutoka nchi za Nigeria na Afrika Kusini.