KENYA-UHURU KENYATTA

Kenyatta akutana na Wabunge kuhusu Tume ya uchaguzi

Rais Uhuru Kenyatta na makamo wake William Ruto,Aprili 4, 2015 Nairobi.
Rais Uhuru Kenyatta na makamo wake William Ruto,Aprili 4, 2015 Nairobi. REUTERS/Thomas Mukoya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anaongoza mkutano wa Wabunge wa serikali kuteua majina ya wajumbe watakaoketi katika Kamati maalum ya kutatua mzozo wa Tume ya uchaguizi IEBC.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya Rais Uhuru Kenyatta, kutangaza mpango mahsusi utakaosaidia kupatikana kwa suluhu.

Akizungumza kwenye ikulu ya Nairobi, rais Kenyatta amesema ataunda kamati maalumu itakayohusisha Bunge la kitaifa na lile la Seneti, na kwamba kamati hiyo itakuwa na jukumu la kukusanya maoni na kupendekeza njia za kufuata kuhusu shida ya IEBC na si vinginevyo.

Tangazo la rais Kenyatta linaongeza shinikizo zaidi kwa kinara wa muungano wa Cord, Raila Odinga, kukubali kurejea kwenye meza ya mazungumzo baada ya juma hili kutangaza kuendelea na maandamano yao licha ya kupigwa marufuku na polisi.

Rais Kenyatta amewataka viongozi wa Cord kuheshimu hatua anazochukua kumaliza tofauti zao, na kwamba hii ndio njia pekee kulinusuru taifa lao kutumbukia kwenye machafuko.

Viongozi wa Cord wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, watakutana na viongozi wa dini kuzungumzia kile walichoafikiana na rais Kenyatta na namna Cord inavyoweza kushiriki vyema kwenye mchakato huu.