KENYA-UHURU KENYATTA-CORD

Serikali ya Kenya mbioni kupatia ufumbuzi madai ya upinzani

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Nairobi, Julai 21 mwaka 2015.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Nairobi, Julai 21 mwaka 2015. REUTERS/Noor Khamis

Serikali ya Jubilee na muungano wa Cord nchini Kenya, hapo jana wameanza mchakato unaotarajiwa kuwa huenda ukatoa matokeo mazuri kushughulikia madai ya upinzani unaotaka kufanyika kwa uteuzi mpya wa wajumbe watakaoshiriki mazungumzo na sio kutumia njia ya bunge.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo viongozi wa pande zote mbili walishindwa kukubaliana njia ya kuendelea mbele, baada ya muungano wa Jubilee kudai kuwa madai ya Cord kutaka kuwa na timu ya watu wanne pekee hayana msingi kwakuwa Serikali imeonesha utayari wa kumaliza mzozo uliopo.

Knara wa muungano wa upinzani Kenya (CORD), Raila Odinga, mbele ya wafuasi wake, wakati wa maandamano Kisumu, Juni 6, 2016.
Knara wa muungano wa upinzani Kenya (CORD), Raila Odinga, mbele ya wafuasi wake, wakati wa maandamano Kisumu, Juni 6, 2016. REUTERS/Thomas Mukoya

Kinara wa CORD, Raila Odinga ameendelea kusisitiza kuwa hakutakuwa na muafaka ikiwa baadhi ya masuala yao waliyoyaibua baada ya tangazo la rais hayatashughulikiwa ili kutoa mwanya wa kuanza kwa mazungumzo.

Kwa upande wake rais Uhuru Kenyatta, ameendelea kusisitiza ufuatwaji wa sheria za nchi kwenye kutatua mzozo wa IEBC, huku akivikosoa baadhi ya vyombo vya habari ambavuo anasema kazi yao imekuwa ni kukosoa na kujaribu kuwagawa wananchi kitu ambacho haungi mkono.

Viongozi wa CORD hata baada ya kukutana na viongozi wa dini, bado wameendelea kusisitiza msimamo wao wa kutotumia bunge na badala yake wanataka utumike mfumo uliotumika kupata suluhu ya mara baada ya machafuko ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008.