BURUNDI-NKURUNZIZA

Burundi: wanafunzi zaidi ya 230 wafukuzwa

Shule ya Carolus-Magnus-Schule (Charlemagne), Kajaga, Burundi.
Shule ya Carolus-Magnus-Schule (Charlemagne), Kajaga, Burundi.

Wanafunzi 239 wa shule ya sekondari ya Gahinga wilayani Gisuru mkoani Ruyigi, mashariki mwa Burundi, wamefukuzwa shule wakituhumiwa kuharibu picha ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Matangazo ya kibiashara

Visa vya kuharibu picha ya Rais Nkurunziza vinaendelea kuripotiwa kwa wingi katika shule mbalimbali nchini humo. Baada ya mkoa wa Muramvya, katikati mwa Burundi, ambapo wanafunzi kumi na mmoja wa shule ya sekondari kukamatwa wakituhumiwa kuharibu picha ya Rais Nkurunziza kwenye vitabu, huku wanafunzi wawili wakijeruhiwa na mpita njia mmoja kuuawa ambapo wanafunzi walikua wakiandamana wakipinga kukamatwa kwa wanafunzi hao, visa hivyo vimeendelea kushuhudiwa katika shule mbali za mikoa tofauti ya nchi ya Burundi.

Kwa sasa visa hivyo vya kuharibu picha ya Rais Nkurunziza kwenye vitabu vya shule vimeendelea kushuhudiwa katika mikoa ya Ruyigi na Cankuzo.

Wazazi wa wanafunzi waliofukuzwa shule mkoani Ruyigi wamelaani mwenendo wa viongozi wa shule kuchukua hatua bila kuwashirikisha, wakisema kwamba huenda watoto zao walizingiziwa.

Kiongozi wa shule ya sekondari ya Gahinga, Guillaume Kwizera amethibitisha taarifa hiyo ya kufukuzwa kwa wanafunzi hao, akibaini kwamba mwenendo huo potovu unaondelea kushuhudiwa katika shule mbalimbali za sekondari unamdhalilisha Rais wa Pierre Nkurunziza.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza. AFP/Carl de Souza

Wakati hayo yakijiri muda uliyotolewa na Rais Pierre Nkurunziza wa kuyataka makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao katika wilaya ya Mugamba mkoani Bururi, kusini mwa nchi hiyo, kurejesha silaha unakwisha leo Jumatano.
Viongozi mbalimbali nchini humo wanatarajiwa leo Jumatano kutoa hotuba mbalimbali za kuyataka makundi hayo kurejesha silaha, la sivyo serikali itumiye nguvu.

Hali ya usalama inaendelea kudorora nchini Burundi, ambapo hivi karibuni watu kadhaa waliuawa katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na mwanajeshi ambaye aliuawa kwa guruneti aliyokua nayo. Inasemekana kwa mwanajeshi huyo alikua akijianda kuirusha guruneti hiyo katika kundi la watu.