BURUNDI-MKAPA

Mkapa anyooshewa kidole na baadhi ya wanaharakati

Askari wa Burundi wakipiga doria katika mtaa mmoja Bujumbua, Aprili 12, 2016.
Askari wa Burundi wakipiga doria katika mtaa mmoja Bujumbua, Aprili 12, 2016. STRINGER / cds / AFP

Mashirika ya kiraia nchini Burundi, yanasema hawana imani na mratibu wa mazungumzo ya amani nchini humo rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati hao wanaotetea watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, wanasema uamuzi wao unakuja baada ya mratibu huyo kukutana na muungano wa vyama vya upinzani CNARED jijini Brussels nchini Ubelgiji.

Wanakosoa hatua ya Mkapa kukutana na wapinzani hao kwa madai kuwa wao ndio chanzo cha ukosefu wa amani nchini mwao.

Hayo yakijiri watu zaidi ya ishirini wamekamatwa na polisi mapema Alhamisi hii asubuhi mtaani Kanyosha, kusini mwa mji mkuu Bujumbura. Mpaka sasa polisi haijafahamisha sababu za kukamatwa kwa watu hao.

Hata hivyo raia mjini Bujumbura wanaendelea kutiwa wasiwasi ikiwa zimesalia siku mbili ili kongamano kuu la chama tawala lifanyike. Wakazi wa mji wa Bujumbnura wana hofu kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi kutokana na kongamano hilo, ambapo tayari kumeanza kujitokea mgawanyiko katika chama hicho. Baadhi ya wafuasi wa chama cha CNDD-FDD wanasema muhula wa miaka minne wa kiongozi wa chama hicho Pascal Nyabenda ambao ungemalizika mwaka 2017, umefupishwa kwa sababu zisizoeleweka.