UGANDA - BESIGYE

Besigye aomba kuachiwa kwa dhamana

Kiongozi wa upinzani Uganda, Kizza Besigye.
Kiongozi wa upinzani Uganda, Kizza Besigye. © AFP PHOTO / ISAAC KASAMANI

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani nchini Uganda cha FDC, Dr Kizza Besigye, amewasilisha jalada kwenye mahakama kuu ya jijini Kampala, akiomba kupatiwa dhamana.

Matangazo ya kibiashara

Besigye, ambaye kwa sasa anashikiliwa kwenye gereza la Luzira akikabiliwa na mashtaka ya uhaini baada ya kutangaza kujiapisha mwenyewe jkama rais wa Uganda, aliwasilisha maombi ya kupatiwa dhamana June 7.

Besigye ambaye kwenye maombi yako alitumia anuani ya gereza la Luzira kama makazi yake, aliandika sababu 10 kwa mahakama kwanini ikubali kumuachia kwa dhamana, ikiwemo kufikisha umri wa miaka 60 na kutoingilia upelelezi unaoendelea dhidi yake.

Haya yanajiri wakati huu ambapo juma hili, mahakama kuu iliukatalia upande wa mashtaka kuhamisha kesi ya Besigye kutoka jijini Kampala.

Kiongozi wa upinzani Dr. Kizza Besigye akiwa na wafuasi wake kwenye eneo la Rukungiri, jijini Kampala, 18 fébruary 2016
Kiongozi wa upinzani Dr. Kizza Besigye akiwa na wafuasi wake kwenye eneo la Rukungiri, jijini Kampala, 18 fébruary 2016 REUTERS/Edward Echwalu

Uamuzi wa Besigye kuomba kupatiwa dhamana umekuja baada ya majuma kadhaa ya kushuhudia kesi yake ikiahirishwa mahakamani kwa kile upande wa mashtaka unadai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Uganda wameiambia mahakama kuwa, Besigye hana vigezo vya kupewa dhamana kutokana na kosa lenyewe pamoja na uwezekano wa yeye akiwa nje kuingilia upelelezi unaoendelea.

Vyama vya upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Uganda, zinakosoa mfumo wa mahakama kuingiliwa na mamlaka za Serikali, ambapo wanadai kuwa maamuzi yanayotolewa na majaji kwenye kesi hiyo, yamekuwa ya kuegemea upande wa Serikali.

Mara kadhaa wabunge wa upinzani wamekuwa wakishinikiza Serikali kumuachia huru Besigye, ambapo wakati wa usomwaji wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, wabunge hao waliingia na mabango na kupiga kelele kumtaka rais Museveni amuachie huru.