MOMBASA - KENYA

Wanaharakati wakosoa uamuzi wa mahakama ya Mombasa

Jengo la mahakama kuu mjini Mombasa, Kenya
Jengo la mahakama kuu mjini Mombasa, Kenya RFI

Mahakama nchini Kenya imetupilia mbali pingamizi lililokuwa limewasilishwa kupinga mtu mmoja kufanyiwa uchunguzi wa njia ya haja kubwa kubaini ikiwa alikuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja au la.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa mahakama kutupilia mbali pingamizi hili, umekosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yanasema kuwa kuruhusu Polisi kufanya uchunguzi huo unaenda kinyume na haki za binadamu.

Kesi hiyo iliwasilishwa na watu wawili waliopinga hatua ya Polisi kuomba mahakama kuruhusu mtuhumiwa kufanyiwa vipimo vya sehemu ya haja kubwa ili kuwasaidia kujua ikiwa alikuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja au la.

Jaji Anyara Emukule wa mahakama kuu ya mjini Mombasa, akisoma uamuzi wake, amesema kuwa Polisi haikuwa na njia nyingine kuthibitisha ikiwa mtuhumiwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja au la, ila kwa kumfanyia vipimo vya sehemu yake ya haja kubwa.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, mtu anayebainika kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja atakabiliwa na kifungo cha miaka 14 jela licha ya kuwa hakuna kesi nyingi zinazohusu ushoga kwenye taifa hilo.

Mtuhumiwa ameruhusiwa kukata rufaa kupinga kufanyiwa uchunguzi huo.