Kenya

Wabunge 8 wa Kenya waachiwa huru kwa dhamana

RFI

Mahakama jijini Nairobi imeaachilia huru kwa dhamana Wanasiasa wanane wa Kenya walioshitakiwa siku ya Ijumaa kwa matamshi ya chuki na kuchochea ghasia kufuatia maoni waliyoyatoa mbele ya umma.

Matangazo ya kibiashara

Wabunge hao watatu ni kutoka chama tawala cha Jubilee, na wabunge wanne na Seneta mmoja ni kutoka muungano wa upinzani CORD, ambapo hata hivyo walikana mashtaka hayo katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi.

Video moja iliyowekwa mitandaoni mwishoni mwa juma lililopita, ilimuonesha mbunge wa chama tawala cha Jubilee, Moses Kuria, akitoa wito wa kuuawa kwa kinara wa muungano wa upinzani ODM Raila Odinga, Kauli ambayo hata hivyo Kuria ameikanusha.

Wabunge wengine wa chama tawala wanaokabiliwa na mshtaka hayo ya uchochezi ni Ferdinand Waititu (Kabete) na Kimani Ngunjiri (Bahati).

Kwa upande wa muungano wa upinzani-CORD ni seneta wa jimbo la Machakos Johnson Muthama wabunge Junet Mohamed (Suna East), Timothy Bosire (Kitutu Masaba), na wawakilishi wa wanawake Aisha Jumwa (Kilifi ) na Florence Mutua (Busia ) ambao walijibu matamshi hayo, huku wakiwaomba wafuasi wao kumlinda bwana Odinga.

Wanasiasa hao waliachiwa hapo jana baada ya kukamatwa na kuziliwa kwa siku nne kabla ya kufikishwa mbele ya mahakama.
Kwa upande mwingine kinara wa upinzani raila Odinga amesema amemsamehe na hana kinyongo na mbunge wa Jubilee Moses Kuria ambaye alitamka kuwa kiongozi huyo anastahili kuuawa.