KENYA

Shambulizi la gruneti lamuua mtu mmoja Garissa nchini Kenya

Gari la kuwabebea wagonjwa
Gari la kuwabebea wagonjwa abc news

Mtu mmoja ameuawa baada ya gari la wagonjwa kukanyaga gruneti iliyokuwa imetegwa ardhini karibu na mji wa Hulugho katika Kaunti ya Garissa Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Tukio hili lilitokea Jumatatu jioni, wakati gari hilo lilipokuwa linarejea hospitalini likiwa na mgonjwa.

Ripoti zinasema kuwa watu watatu walijeruhiwa na wanaendelea kupata matibabu lakini dereva wa gari hilo alipoteza maisha papo hapo.

Mwakilishi wa serikali katika eneo hilo la Kaskazini Mashariki, Mohamud Saleh amethibitisha na kulaani shambulizi hilo.

Mbali na shambulizi hili, maafisa watano wa polisi walipoteza maisha baada ya gari walilokuwa wanasafiria kulipuliwa na gruneti iliyokuwa imetegwa ardhini, wakati wakilisindikiza basi la abiria katika kaunti ya Mandera.

Miili ya maafisa hao inatarajiwa kusafirishwa jijini Nairobi baadaye hivi leo.

Kenya imeendelea kupambana na ugaidi, tangu mwaka 2011 serikali ya nchi hiyo ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia kupambana na Al Shabab.