TANZANIA

Ugonjwa usiojulikana waua watu 7 Tanzania

Mwonekano wa mbali wa mji wa Dodoma
Mwonekano wa mbali wa mji wa Dodoma Reuters

Wizara ya afya nchini Tanzania imewataka raia wa nchi hiyo hasa wakaazi wa mkoa wa Dodoma kusalia watulivu baada ya kuibuka kwa ugonjwa usiojulikana, ambao Serikali inasema tayari imechukua sampuli, kutoka kwa watu walioathirika kuzifanyia vipimo vya kimaabara kubaini undani wa ugonjwa wenyewe.

Matangazo ya kibiashara

Naibu Waziri wa afya nchini humo Dkt. Hamis Kigwangalla kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema watalaam wa afya wanachunguza kiini cha ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya watu 7 na zaidi ya 20 kulazwa katika hospitali ya mkoa mjini Dodoma.

Madaktari katika hospitali hiyo wanasema, wagonjwa waliolazwa wamekuwa wakitapika, kuharisha, kuumwa tumbo na macho na ngozi kubadilika rangi na kuwa njano.

Wagonjwa hao wamelazwa kwenye wodi maalum, huku juhudi zikifanyika kubaini chanzo cha ugonjwa huu na tiba yake.

Inaelezwa kuwa watu 9 wa familia moja walianza kusumbuliwa na ugonjwa huo baada ya kula nyama ya ng'ombe aliyechinjwa baada ya kuvunjika mguu katika mazingira yasiyoeleweka.