KENYA-EU

Kenya yasema uchumi wake utatikisika ikiwa Uingereza itajiondoa kwenye Umoja wa Ulaya

Jiji kuu la Kenya, Nairobi
Jiji kuu la Kenya, Nairobi http://buzzkenya.com

Kenya inasema itakuwa miongoni mwa nchi mbalimbali duniani zitakazotikisika kiuchumi ikiwa Uingereza itajiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Gavana wa Benki Kuu nchini humo Patrick Njoroge, ambaye pia aliwahi kuwa mmoja wa wachumi wa Shirika la fedha duniani IMF, amesema ni muhimu sana kwa Uingereza kusalia katika Umoja huo ili uchumi wa nchi yake uendelee kuwa imara pamoja na kuendelea kwa biashara.

Watalaam wa uchumi nchini Kenya nao wanasema, makampuni kadhaa yanayosafirisha bidhaa nchini Uingereza, biashara zitayumba ikiwa Uingereza itajitoa.

Aidha, wanaongeza kuwa matokeo ya kujitoa yanaweza kusababisha mzozo wa kiuchumi duniani, uliowahi kushuhudiwa mwaka 2008.

Kenya imekuwa ikituma bidhaa kama maua katika soko la Uingereza chini ya mwafaka wa Umoja wa Ulaya, na kufanya bei ya ufanyaji biashara kuwa rahisi.

Mbali na Kenya, mataifa makubwa kiuchumi duniani kama Marekani, Ufaransa na Ujerumani yamewataka raia wa Uingereza kupiga kura ya kusalia katika umoja huo.

Raia wa Uingereza kesho Alhamisi watafanya uamuzi huo wa kihistoria wa kusalia au kuondoka kwenye umoja huo.