SUDAN KUSINI

UN: Sudani Kusini iwakamate walioshambulia kambi ya wakimbizi

Shambulizi katika kambi ya Malakal mwezi Februari mwaka 2016
Shambulizi katika kambi ya Malakal mwezi Februari mwaka 2016 Justin LYNCH / AFP

Umoja wa Mataifa unaitaka serikali ya Sudan Kusini, kuwajibikia uvamizi uliotokea kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani iliyokuwa inawapa hifadhi zaidi ya watu 50,000 katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Malakal mwezi Februari mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya watalaam wa Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa baada ya uchunguzi wao, wamebaini kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na jeshi la serikali ya Sudan Kusini kati ya tarehe 17 na 18 mwezi huo wa Februari.

Imebainika kuwa wavamizi hao walitumia silaha hatari zikiwemo maguruneti kuwashambulia wakimbizi hao na kusababisha vifo vya watu 30 na wengine 123 kujeruhiwa.

Ushahidi kutoka kwa watu walioshuhudia shambulizi hilo wakiwemo wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wanawahifadhi raia hao, wanasema wavamizi hao waliwalenga watu wa kabila la Nuer na Shilluk na kuwaacha wale kutoka kabila la rais Salva Kiir la Dinka na kabila lingine la Dafuri.

Kambi ya wakimbizi ya Malakal
Kambi ya wakimbizi ya Malakal http://www.eyeradio.org/

Katika hatua nyingine, imebainika kuwa Gavana wa jimbo la Eastern Nile aliwasaidia watu kutoka kabila la Dinka kutoroka mji wa Malakal kwa kutuma malori ya kuwasafirisha.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amewaambia viongozi wa nchi hiyo kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na shambulizi hilo wakiwemo, wanajeshi na viongozi wa kisiasa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litajadili ripoti hii baadaye siku ya Jumatano.