KENYA

Obama ampigia simu Kenyatta kuhusu wakimbizi wa Somalia

Kambi ya wakimbizi ya Daadab kaskazini mwa nchi ya Kenya, inayohifadhi wakimbizi wa Somalia
Kambi ya wakimbizi ya Daadab kaskazini mwa nchi ya Kenya, inayohifadhi wakimbizi wa Somalia UNHCR - kenya

Rais wa Marekani Barrack Obama amempigia simu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kuzungumza naye kuhusu kufungwa kwa kambi ya wakimbizi ya Daadab inayowapa hifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Obama amemwambia Kenyatta umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwasadia wakimbizi wanaoishi katika nchi hiyo.

Ripoti zinasema kuwa viongozi hao wamekubaliana kushirikiana kwa mataifa yao, kuhakikisha kuwa haki za wakimbizi hao zinalindwa na kuheshimiwa.

Kenya imepanga kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa Somalia, kufikia mwisho wa mwaka huu.

Nairobi inasema, sababu kubwa inayowasuma kufikia uamuzi huo ni ya kiusalama baada ya kubainika kuwa, kambi hiyo imekuwa ikitumiwa na wanamgambo ya Al Shabab kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon mjini Brussels, Ubelgiji 15 Juni 2016
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon mjini Brussels, Ubelgiji 15 Juni 2016 Kenya Govt

Wiki iliyopita, rais Kenyatta alikuwa ziarani jijini Brussels nchini Ublegiji na kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na kujadiliana kwa kina kuhusu hatima ya wakimbizi hao.

UN imesema itashirikiana na Kenya, kuhakikisha kuwa wakimbizi hao wanarudi nyumbani katika mazingira mazuri na ya kibinadamu baada ya kuishi nchini humo kwa zaidi ya miaka 20.