KENYA-SIASA

ODM: Tunahujumiwa na wanasiasa wa muungano wa Jubilee

Kinara wa upinzani Raila Odinga (Kushoto) akiwa na katibu mkuu wa chama cha KANU, wanaituhumu Serikali kuwafanyia rafu
Kinara wa upinzani Raila Odinga (Kushoto) akiwa na katibu mkuu wa chama cha KANU, wanaituhumu Serikali kuwafanyia rafu REUTERS/Thomas Mukoya

Sintofahamu ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu nchini Kenya imeendelea kushuhudiwa wakati huu, mzozo mkali ukiripotiwa kufukuta ndani ya chama kikuu cha upinzani cha ODM.

Matangazo ya kibiashara

Mwishoni mwa juma baadhi ya wanasiasa kutoka chama cha ODM, walitangaza kuachana na chama hicho katika kile wakuu wa chama hicho wanasema ni hujuma zinazofanywa na Serikali ya chama tawala.

Vinara wa ODM na wale wanaounda muungano wa Cord, wanaituhumu Serikali kwa kucheza rafu na kuwashawishi kwa nguvu wanasiasa wake muhimu kuasi vyama vyao na kutaka kujiunga na muungano wa Jubilee.

Hata hivyo naibu wa rais wa Kenya, William Ruto, amesema anashangazwa na matamshi ya baadhi ya wanasiasa ndani ya muungano wa upinzani, CORD, kuwa Serikali yake inafanya njama za kuhujumu upinzani wakati huu mzozo ukifukuta ndani ya chama kikuu cha upinzani, ODM.

Kauli ya Ruto, anaitoa wakati huu, ripoti zikidai kuwa kamati ya maadili ndani ya chama cha ODM, itaketi kumjadili katibu mkuu wa chama hicho, Ababu Namwamba, anayedaiwa kwenda kinyume na muongozo wa chama pamoja na kumkosoa kiongozi wa chama Raila Odinga.

Naibu wa rais William Ruto anasema, nyakati hizi sio nyakati za utawala wa kiimla na kwamba kila mtu ndani ya chama chochote kile anao uhuru wa kutoa mawazo yake hata kama mtazamo wake utakera baadhi ya watu.

Haya yanajiri wakati huu, muungano wa upinzani ukiongoza kampeni za nchi nzima kushinikiza kuondoka madarakani kwa makamishna wa tume ya uchaguzi ya IEBC, ambayo wanasema hawatakubali kuona tume ya sasa ikisimamia uchaguzi mkuu ujao.