BURUNDI-AU

Ujumbe wa tume ya umoja wa Afrika, wamaliza ziara Burundi

Burundi, mzunguko wa vurugu na ukandamizaji vinandelea kushuhudiwa kwa mwaka mmoja sasa. Bujumbura, Februari 3, 2016.
Burundi, mzunguko wa vurugu na ukandamizaji vinandelea kushuhudiwa kwa mwaka mmoja sasa. Bujumbura, Februari 3, 2016. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana

Ujumbe wa baraza la amani na usalama wa umoja wa Afrika uliofanya ziara nchini Burundi, umehitimisha ziara yake mwishoni mwa juma, ambapo umesema, licha ya hali kuimarika, bado kuna mengi ya kufanywa kwenye taifa hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Wakizungumza na wandishi wa habari mjini Bujumbura baada ya kumaliza ziara ya siku 2, wajumbe hao wa baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika, wamebaini kuwa wamekusanya habari zote walizokuwa wakihitaji na kwamba watatoa maagizo wakifika Addis Ababa.

Mmoja wa wajumbe waliotembelea nchi hiyo, Makayate Safouesse anasema ziara yao imewasaidia kujua namna hali ya mambo ilivyo nchini Burundi, na kwamba watakaporejea mjini Addis Ababa watakuwa na mengi ya kueleza kwa wakuu wa nchi.

Ama kuhusu mazungumzo baina ya warundi yanayofanyika mjini Arusha chini ya usuluhishi wa rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, amesema ikiwa muungano wa upinzani CNARED na makundi mengine wataweza kushiriki, huenda suluhu ikapatikana mapema zaidi.

Safousesse, amesema ni jukumu la msuluhishi kuzialika pande anazoona zinahusika na zina umuhimu mkubwa kwenye kupata suluhu ya nchi hiyo, na kwamba ikiwa ameona inafaa kuzialika pande ambazo hazikushiriki awali, ni jambo jema.

Ziara hii imefanyika wakati awamu nyingine ya mazungumzo baina ya wadu wa siasa,
Burundi yanatarajiwa kuitishwa mjini Arusha Tanzania mwanzoni mwa mwezi ujao, yote hayo ikiwa ni katika lengo la kutaka kuumaliza mzozo wa kisiasa unaoikabili Burundi, ambao umedumu kwa mwaka mmoja sasa.