UNMISS-SUDANI KUSINI

UNMISS: Tutawalinda raia dhidi ya mashambulizi, Wau

Picha ya maktaba ikiwaonesha baadhi ya raia wa Sudan Kusini wakiwasili kwenye kambi ya umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini iliyoko kwenye mji wa Bor.
Picha ya maktaba ikiwaonesha baadhi ya raia wa Sudan Kusini wakiwasili kwenye kambi ya umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini iliyoko kwenye mji wa Bor. UN Photo/Hailemichael Gebrekrstos

Tume ya umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, imeweka nyenzo maalumu za usalama kuzunguka kambi yake iliyoko kwenye mji wa WAU, kufuatia kuzuka kwa mapigano kati ya wapiganaji wenye silaha na wanajeshi wa Serikali, SPLA.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye taarifa iliyotolewa na UNMISS, imesema kuwa inaendelea kutoa ulinzi kwa zaidi ya raia elfu 1, ambao wamenaswa kwenye mapigano yaliyoanza mwishoni mwa juma.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya kufikiria kwa kina, iliamua kufungua milango yake siku ya Jumapili na kuruhusu mamia ya raia kuingia kwenye kambi yake, wakikimbia mapigano hayo.

Haya yanajiri wakati huu Serikali ya Juba ikitangaza hali ya hatari kwenye mji wa Wau kutokana na kushuhudiwa kwa mapigano ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa ambao mpaka sasa idadi yao haijafahamika.

Katika taarifa iliyotolewa na wakuu wa jimbo la Wau, baada ya kikao cha baraza la usalama la mji huo toka kulipozuka mapigano hayo Jumamosi ya wiki iliyopita, mkuu wa polisi kwenye mji huo, Chol Thuc amesema hali imeanza kurejea kama kawaida.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mapigano kwenye mji huo, ambapo maelfu ya raia wameendelea kuyakimbia makazi yao kwa hofu ya kiusalama.

Mashirika hayo yanautaka umoja wa Mataifa kuingilia kati hali hiyo, kwa kuvisaidia vikosi vya Serikali kukabiliana na makundi ya wapiganaji wenye silaha ambao wameendelea kutekeleza mashambulizi ya kushtukiza kwenye maeneo mengi ya nchi.