TANZANIA

Wanaobaka, kuolewa au kuoa wanafunzi kukiona nchini Tanzania

Picha ya maktaba msichana raia wa Afrika ambao wanatetewa kupata elimu
Picha ya maktaba msichana raia wa Afrika ambao wanatetewa kupata elimu DR

Bunge la Tanzania, limepitisha sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba 2 ya mwaka 2016, ambapo limeongeza adhabu kwa watu wanaowapa mimba wanafunzi, kuoa au kuolewa na wanafunzi, ambapo sasa watahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Matangazo ya kibiashara

Sheria hii imepitishwa baada ya muswada wa marekebisho yake kuwasilishwa bungeni Juni 24 mwaka huu na mwanasheria mkuu wa Serikali, ambapo wabunge walipata nafasi ya kuchangia mawazo yao kabla ya kupitishwa.

Muswada huu ulilenga kufanya marekebisho katika sheria ishirini na moja (21) kwa lengo la kuondoa mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezwaji wa sheria hiyo na sheria nyingine, ambapo sasa umepitishwa kuwa sheria.

Miongoni mwa sheria nyingine zinazohusu haki za binadamu zilizfanyiwa marekebisho na kuongezewa adhabu, ni pamoja na usafirishaji haramu wa Binadamu na Elimu.

Akizungumza bungeni wakati akijibu maswali yaliyoulizwa na wabunge kuhusu mapungufu yaliyokuwepo awali na namna marekebisho ya sheria hii yatakavyofanikisha utekelezwaji wake, mwanasheria mkuu wa Serikali George Masaju, alisema sheria hii sasa inatamka kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho ya elimu kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania
Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania RFI

Awali mtu aliyekuwa akipatikana na hatia ya makosa haya, aliadhibiwa kulipa faini ya shilingi za Tanzania laki tano (500,000) au kifungo kisichopungua miaka mitatu.

Masaju amesema sheria hii inawalinda watoto wote wa chini ya miaka 18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.

Kifungu cha 60 A kipengele cha i, kimeeleza kuwa,itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari ay ya msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.

Baadhi ya wadau na wanaharakati wa haki za binadamu walioongea na idhaa ya Kiswahili ya Radio France International, wamepongeza kupitishwa kwa muswada huu wa sheria ambao sasa unasubiri saini ya Rais ili kuwa sheria rasmi.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Idhaa hii, mmoja wa wadau wa haki za binadamu nchini Tanzania, James Mlali, amesema "kupitishwa kwa muswada huu bungeni kunaonesha wazi nia njema ya Serikali na sheria yenyewe kuhusu kuwaadhibu watu wanaofanya kosa hili." alisema Mlali.

Aidha ametoa angalizo kwa watekelezaji na wasimamizi wa sheria yenyewe, kwamba kwa sehemu pia mila na tamaduni zilizopitwa na wakati zinachangia pakubwa kwa jamii fulani kuwaficha watu wanaofanya au waliowahi kufanya vitendo hivi.