UGANDA

Besigye kujisimamia mwenyewe mahakamani

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, ambaye anaendelea kushikiliwa kwenye gereza la Luzira nchini Uganda.
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, ambaye anaendelea kushikiliwa kwenye gereza la Luzira nchini Uganda. AFP PHOTO / ISAAC KASAMANI

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini, hii leo anatarajiwa kupandishwa tena kizimbani kwenye mahakama ya Uganda, ambapo atajiwakilisha mwenyewe bila ya mawakili wake.

Matangazo ya kibiashara

Besigye ambaye toka kushikiliwa kwake ameshapandishwa kizimbani kwenye mahakama kadhaa za Uganda, kwenye maeneo tofauti tofauti ya nchi, hali ambayo mawakili wake wanasema wanashindwa kumuwakilisha vema.

Hivi leo Besigye anatarajiwa kupanda kizimbani bila kuwa na mawakili wake, katika kile alichosema ni hujuma zinazofanywa dhidi yake kuhakikisha anakosa wawakilishi muhimu kwenye kesi ambayo ameendelea kusisitiza kuwa imepikwa kisiasa kumaliza.

Mmoja wa mawakili wake, YUSUF NSIBAMBI, akizungumza na idhaa ya RFI, amesema wao kama wataalamu wa sheria wanashindwa kumuwakilosha Besigye inavyopaswa kutokana na kutokuwepo kwa mahakama moja inayosikiliza kesi yake, na kwamba wanaona ni kama tayari ameshahukumiwa kuliko madai ya Serikali kuwa anashtakiwa.

Wafuasi wa Besigye, wanaharakti pamoja na wanasiasa wengine nchini Uganda, wamekosoa namna kesi hiyo inavyoendeshwa wakisema siasa imeingia hadi kwenye mfumo wa kimahakama, kwakuwa kiongozi huyo hapati haki yake kisheria kama inavyotamkwa kwenye katiba ya nchi.

Besigye mwenyewe ameendelea kushikilia msimamo wa kujiwakilisha mwenyewe hii leo, kwa kile anachosema ni kudai haki yake popote pale atakaposomewa mashtaka hata kama sio kwenye mahakama moja inayofahamika.