KENYA

Odinga katika mtihani wa kukiunganisha chama chake cha ODM

Raila Odinga, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Kenya, ODM.
Raila Odinga, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Kenya, ODM. REUTERS/Noor Khamis

Kamati ya uongozi ya chama kikuu cha upinzani nchini Kenya, ODM, hii leo inakutana kujadili mustakabali wa chama hicho kisiasa pamoja na kutafuta suluhu ya mgawanyiko unaofukuta ndani ya chama baina ya viongozi wa juu.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya ajenda kubwa ya kikao cha leo kuwa ni kupitiwa na kufanyiwa marekebisho kwa kamati ya uchaguzi ya ndani ya chama, wadadisi wa mambo wanasema kikao hicho pia kitajadili mtafauruku uliojitokeza kati ya uongozi wa chama na baadhi ya wabunge wanaotoka eneo la pwani.

Kiongozi wa chama, waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, anakabiliwa na changamoto kubwa ya kukiunganisha chama chake ambacho ni wazi kimeanza kushuhudia mgawanyiko na mitafuruku ya ndani kwa ndani, kuanzia kwa katibu mkuu wake Ababu Namwamba na makamu mwenyekiti wa chama Paul Otuoma.

Odinga anadaiwa kuwa alifanya mawasilino na baadhi ya waliokuwa viongozi wa chama hicho pamoja na wale wanaoraka kukiasi chama, ikiwa ni katika jitihada zake za kujaribu kumaliza mpasuko unaokinyemelea chama hicho wakati huu kikijiandaa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.

Wanasiasa kindakindaki wa chama wanaona kuwa katibu mkuu Ababu Namwamba anamsaliti kiongozi wa chama Raila Odinga, na kwamba ikiwa suluhu haitapatikana kuna wasiwasi kuwa kiongozi huyo atahamia upande wa pili wa muungano wa chama tawala cha Jubilee.