BURUNDI-UN

Al-Hussein: Serikali na upinzani wanahusika na mauaji Burundi

Zeid Ra’ad Al-Hussein, kamishna mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa.
Zeid Ra’ad Al-Hussein, kamishna mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa. UN Photo/Jean-Marc Ferré

Watu zaidi ya 348 wamekufa nchini Burundi kutokana na mauji ya kupangwa yanayoendelea kutekelezwa kwenye taifa hilo lililoko kwenye mzozo wa kisiasa toka mwezi April mwaka 2015, amesema mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa.

Matangazo ya kibiashara

Mauaji hayo kwa sehemu kubwa yamedaiwa kutekelezwa na Polisi, usalama wa taifa, polisi wa kutuliza ghasia na wapiganaji wenye uhusiano na chama tawala cha CNDD-FDD, alisema Zeid Ra’aad Al Hussein, mkuu wa tume ya haki za binadamu.

Mbali na Serikali kulaumiwa kutekeleza mauaji hayo, tume hiyo pia imeainisha mauaji ya watu zaidi ya 134 waliouawa na makundi ya wapiganaji yenye uhusiano na makundi yanayodaiwa kuupinga utawala wa rais Pierre Nkurunziza.

Nchi ya Burundi imejikuta ikitumbukia kweye machafuko ya kisiasa toka rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu mwezi April mwaka 2015, ambapo alichaguliwa tena mwezi Julai kwenye uchaguzi uliosusiwa na upinzani.

Machafuko nchini humo yamesababisha watu zaidi ya laki 2 na elfu 70 kuikimbia nchi yao, na kuzusha hofu ya kuenea kwa machafuko zaidi kwenye nchi za maziwa makuu, huku mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda yakifanana na mzozo unaofukuta Burundi.

Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, tume ya haki za binadamu ilirekodi matukio zaidi ya 651 ya watu kuteswa.

Matukio haya yanaripotiwa kutekelezwa kati ya mwezi April na Julai mwaka 2015 na kutoka mwezi December hadi April 2016, kipindi ambacho matukio ya wapinzani kuminywa yalikithiri, imesema ripoti.

Umoja wa Afrika umepanga kutuma wanajeshi zaidi ya 200 na waangalizi wa haki za binadamu kwenda nchini Burundi, kusaidia kutuliza mzozo wa kisiasa. Hata hivyo askari hao na wanajeshi bado hawajatumwa kikamilifu.