BURUNDI-TANZANIA

Wakati Burundi ikiadhimisha siku ya Uhuru, CNDD-FDD yaeleza msimamo wake

Wakati taifa la Burundi likiadhinisha kumbukumbu ya miaka 54 ya Uhuru wake Julai Mosi kutoka mikononi mwa mkoloni Ubelgiji, Chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD kimetoa taarifa na kueleza msimamo wake kuhusu kile kinachoitwa mazungumzo mapya ya Arusha. 

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza REUTERS/Evrard Ngendakumana
Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliosaniwa na mwenyekiti wa chama hicho Pascal Nyabenda na kusomwa na katibu wake Daniel Gelase Ndabirabe, amesema ukweli unaosubiriwa na Warundi kuhusu amani ya Burundi hautotoka kwenye mazungumzo mengine ya Arusha.

Ndabirabe amesisitiza kuwa wadau wa kisiasa wanaotaka kushiriki kwenye mazungumzo hayo ndio hao hao walioshiriki kwenye mazungumzo ya Arusha One mwaka 2000, ambao wengi miongoni mwao wanagubikwa na sifa ya uongo na wenye kutafuta maslahi binafsi.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, aliyetembelea nchi ya Burundi hivi karibuni akizungumza huku akisikilizwa na mwenyeji wake Pierre Nkurunziza
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, aliyetembelea nchi ya Burundi hivi karibuni akizungumza huku akisikilizwa na mwenyeji wake Pierre Nkurunziza AFP

Taarifa hiyo ya chama tawala imeendelea kuwa, mwaka 2000 kundi la warundi walielekea Arusha nchini Tanzania kwa ajili ya mazungumzo bila kutumwa na wananchi kwa ajili ya kutetea maslahi yao, jumui ya Kimataifa na Ubelgiji wakafadhili na ndipo ukapatikana mkataba wa amani wa Arusha.

Kundi hilo hilo la waliokwenda Arusha mwaka 2000 ndio ambao wanataka kuwepo kwa Arusha namba 2, sababu hawakunufaika na kile walichokuwa wakitetea, na hili limedhihirika Mei 13 mwaka 2015 pale walipotaka kuungusha utawala uliochaguliwa katika misingi ya Kidemokrasia.

Chama tawala nchini Burundi kinaona kuwa hakuna sababu za kuwepo kwa makubaliano mapya ya Arusha, bali kinachotakiwa na makubaliano ya wananchi hasa wale wa vijijini wakiwemo wazee ambao watajadili kwa kina kiini cha mzozo na kupata suluhu ya kudumu.

Polisi wa Burundi wakifanya doria kwenye jiji la Bujumbura, hivi karibuni
Polisi wa Burundi wakifanya doria kwenye jiji la Bujumbura, hivi karibuni AFP PHOTO / SIMON MAINA

Tuhuma zimeelekezwa kwa viongozi wa kanisa katoliki nchini Burundi ambao wameonekana kuegemea upande mmoja na ambapo wamegeuka kuwa wanasiasa badala ya kuwa wachungaji na kuwaongoza waumini kiimani, hata mwaka 2000 walipewa nafasi pia katika mazungumzo.

Taarifa hii ya chama tawala imepingwa vikali na upinzani ambao unaona kwamba serikali ya chama cha CNDD-FDD unalenga kuwagawa wananchi wa taifa hilo katika misingi ya kikabila, huku mkataba wa Amani wa Arusha ukiminywa, jambo ambalo upinzani unaona kwamba ni hatari katika mustakabali wa taifa.