RWANDA-UFARANSA

Mauaji ya Kimbari Rwanda; Ngezi na Barahira wahukumiwa kifungo cha maisha jela

Mchoro ukionesha kesi ya Tito Baharira na Octavien Ngenzi, ikiendelea jijini Paris, May 10, leo wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mchoro ukionesha kesi ya Tito Baharira na Octavien Ngenzi, ikiendelea jijini Paris, May 10, leo wamehukumiwa kifungo cha maisha jela. BENOIT PEYRUCQ / AFP

Katika hukumu ya kihistoria, mahakama moja jijini Paris, Ufaransa, imewahukumu kifungo cha maisha jela, watu wawili waliowahi kuwa Mameya nchini Rwanda, wakituhumiwa kushiriki na kupanga mauaji ya mamia ya watu wa jamii ya Watutsi, wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. 

Matangazo ya kibiashara

Mahakama imesema kuwa, Octavien Ngezi, mwenye umri wa miaka 58 na mtangulizi wake Tito Barahira, mwenye umri wa miaka 64, walikuwa na hatia ya "makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu", "kupanga njama na kutekeleza mauaji ya kupangwa" pamoja na "mauaji ya kimbari", matendo waliyoyafanya kwenye kijiji Kabarondo, ambako watu wanaofikia elfu 2 waliokuwa wakiomba hifadhi kwenye kanisa moja walichinjwa na wengine kunyongwa.

Ngezi na Barahira, mara zote wamekuwa wakikanusha kuhusika na tuhuma dhidi yao, ambapo wote walionekana kutokuwa na wasiwasi wakati jaji akisoma hukumu.

Hukumu hii, ilikuwa ni hukumu ya juu kabisa kutolewa kwa washukiwa wa mauaji ya kimbari, kutolewa na mahakama ya Ufaransa, ambapo mwaka 2014, kapteni wa zamani kwenye jeshi la Rwanda, Pascal Simbikangwa, alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela, kwa kuhusika kwake na mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.

Kesi hiyo iliyodumu kwa wiki 8, ilipokea ushahidi wa kina na wakusikitisha, ukiwahusisha watu hawa wawili kama wasimamizi wakuu na watekelezaji wa mauaji hayo, ambayo watu zaidi ya laki 8 waliuawa, wangi wakiwa ni jamii ya Watutsi waliouawa na Wahutu.

Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa "Ngezi alikuwa kiongozi" na kuiomba mahakama iwahukumu wote wawili kifungo cha maisha jela, ambapo aliongeza kuwa Barahira alikuwa "mchinjaji".

Mawakili wa Ngezi na Barahira, awali waliionesha mahakama namna ushahidi wa upande wa mashtaka ambavyo ulitofautiana, kutoka kwa mashahidi wao 22 walioletwa mbele ya mahakama, wakitaka kuonesha kuwa wateja wao hawakuwa na uwezo wowote wakati huo wa kuzuia mauaji yasitokee.

Wakili wa Barahira, Philippe Meilhac, ameeleza kuskitishwa kwake na uamuzi wa mahakama, huku akisema kuwa hata hivyo hakushangazwa na kwamba wamepanga kukata rufaa.

Mawakili wa wahanga wa mauaji hayo waliiambia mahakama kuwa "kuua mtu mmoja chuki inaweza kuonekana. Lakini kuua watu zaidi ya elfu 1, unahitaji kuwa na mtandao."