KENYA-SIASA

Namwamba ajiuzulu Ukatibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya ODM

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga (Kushoto), na Ababu Namwamba (Kulia) Katibu Mkuu
Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga (Kushoto), na Ababu Namwamba (Kulia) Katibu Mkuu rao.co.ke

Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya Orange Democratic Movement ODM, Ababu Namwamba ametangaza kujiuzulu.

Matangazo ya kibiashara

Namwamba amesema amechukua hatua hiyo baada ya kushauriana na wazee wa eneo bunge lake la Bundalangi Magharibi mwa nchi hiyo.

Aidha, amemshtumu kiongozi wa chama hicho aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kumsaliti lakini pia viongozi wengine wa chama hicho kumdharau.

Wiki kadhaa zilizopita, alidai kutopewa ushirikiano ndani ya chama hicho na kuongeza kuwa yeye kama msemaji mkuu wa chama amekuwa hapewi ushirikiano.

Wiki iliyopita, Namwamba na viongozi wengine wa chama walikutana katika makao makuu ya chama hicho Orange House jijini Nairobi wakiongozwa na kiongozi wao Odinga na kukubaliana kupata mwafaka baada ya wiki mbili.

Raila Odinga kiongozi wa chama cha ODM

Hata hivyo, viongozi wa chama hicho amekanusha madai ya Namwamba, na kusema kuwa huenda ameshawishiwa kuungana na muungano wa chama cha Jubillee kilicho madarakani huku wengine wakidai amehongwa madai ambayo mbunge huyo ameyakanusha.

Profesa Larry Gumbe mmoja wa viongozi wa chama hicho ameimabia RFI Kiswahili kuwa yeye hajashangazwa na hatua ya Namwamba kwa sababu alikuwa ameonesha nia ya kuondoka katika chama hicho.

“Sijashangazwa na hatua hii kwa sababu hiki kilitarajiwa sana, amekuwa akishirikiana na Ruto (Naibu rais) na huenda anataka kujiunga naye,” alisema Profesa Gumbe.

Aidha, amesema kuwa huu ni wakati wa wanasiasa kuhama vyama kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Naibu Mwenyekiti wa chama hicho Paul Otuoma naye alijiuzulu wiki iliyopita kwa madai kuwa amekuwa hashirikishwi katika maswala ya chama.