KENYA-SOMALIA

Al Shabab wavamia kituo cha polisi nchini Kenya

Polisi nchini Kenya leo Jumamosi imesema kwamba zaidi ya wapiganaji 100 wa Kiislamu wamevamia kituo cha polisi Kaskazini-Mashariki mwa Kenya na kujeruhi afisa mmoja na kuondoka na silaha na risasi.

Wanamgambo wa Al Shabab wa Somalia
Wanamgambo wa Al Shabab wa Somalia AFP / M. Dahir
Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hilo katika kituo cha polisi cha Diff katika wilaya ya Wajir, karibu na mpaka wa Somalia, limetokea majira ya saa nne usiku jana Ijumaa na linadaiwa kufanywa na wapiganaji wa Al Shabaab, kutoka Somalia.

Mkuu wa polisi Joseph Boinnet amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo na kuysema kuwa maafisa waliweka upinzani mkali na kuwafukuzia mbali licha ya wapiganaji hao kuwa zaidi ya 100 wakiwa katika malori matatu na wakiwa na silaha nzito.

Kituo cha polisi cha Diff kilikumbwa na shambulio kama hili mwezi Aprili mwaka huu wakati maafisa watatu walipojeruhiwa na gari la polisi kuibiwa ambapo viongozi walisema wapiganaji karibu 100 wa Al Shabaab walishiriki pia katika uvamizi huo.