KENYA-SOMALIA

Kenya yakanusha ripoti ya UN kuhusu mauaji ya raia wa Somalia

Kenya imekanusha ripoti ya Umoja wa Mataifa kuwa jeshi lake liliwauawa raia wa kawaida 29 wa Somalia baada ya kushambulia eneo la El  Adde mwezi Januari mwaka huu, muda mfupi baada ya wanajeshi wake kuvamiwa katika kambi yao na kundi la Al Shabab.

Wanajeshi wa Kenya wakilinda usalama nchini Somalia
Wanajeshi wa Kenya wakilinda usalama nchini Somalia AFP/AU-UN/Stuart Price
Matangazo ya kibiashara

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa pia imewashtumu wanajeshi wa Kenya kwa kuharibu makaazi ya raia hao na kushambulia na kuua mifugo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ndiye aliyewasilisha ripoti hii mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Moon amewaambia wajumbe hao kuwa baada ya kukutana rais wa Kenya Uhuru Kenyatta mwezi uliopita jijini Brussels nchini Ubelgiji, alikanusha madai ya ripoti hiyo.

Mbali na ripoti hii ya mauaji, jeshi la Kenya pia limekuwa likishtumiwa kwa kujihusisha na  biashara haramu ya kuuzaji wa sukari na mkaa kwa njia za kimagendo katika mji wa Kismayo, madai ambayo jeshi limeendelea kukanusha.

Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyotuma wanajeshi wake zaidi ya 4,000 nchini Somalia kukabiliana na Al Shabab mwaka 2011.