Sudan Kusini yaadhimisha miaka 5 ya uhuru kwa hofu
Imechapishwa:
Milio ya risasi ilisikika karibu na Ikulu ya Sudan Kusini jijini Juba hapo jana siku moja, baada ya wanajeshi watano wanaomtii rais Salva Kiir kuuliwa na wale wanaomtii Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar.
Ripoti kutoka Juba zinasema rais Kiir na Machar walikuwa wanajiandaa kuzungumza na wanahabari wakati milio hiyo ilipoanza kusikika bila kutarajiwa.
Hata hivyo, viongozi hao waliendelea na mkutano huo huku rais Kiir akisema kilichokuwa kinaendelea nje ya Ikulu hangeweza kukielezea.
Rais Kiir na Makamu wake Machar, tangu kuanza kutawala pamoja wamekuwa wakitoa wito wa utulivu kipindi hiki cha mpito kujaribu kurejesha amani nchini humo baada ya kumaliza vita vya miaka miwili.
Yote haya yanatokea Sudan Kusini ikiadhimisha miaka mitano ya uhuru wake baada ya kujitenga rasmi na Sudan mwaka 2011.
Sherehe za leo hazitakuwa na shamrashamra zozote kwa kile serikali ya Juba inasema haina pesa baada ya nchi hiyo kuingia kwenye machafuko mwaka 2013.
Rais Salva Kiir anatarajiwa kulihotubia taifa kupitia runinga baadaye leo.