SUDAN KUSINI

Zaidi ya wanajeshi 100 wa Sudan Kusini wauawa

Wanajeshi wa Sudan Kusini
Wanajeshi wa Sudan Kusini Channel4.com

Uhuru wa miaka mitano wa Sudan Kusini umetawaliwa na huzuni baada ya ripoti ya kuuawa kwa zaidi ya wanajeshi 100 wanaomtii rais Salva Kiir na Makamu wake wa kwanza wa rais Riek Machar jijini Juba.

Matangazo ya kibiashara

Ni siku ambayo ilipaswa kuwa ya furaha kwa raia wa nchi hiyo baada ya uhuru wake 2011 kutoka Sudan, imewakumbusha machungu ya miaka miwili iliyopita baada ya kutokea kwa makabiliano haya nje ya Ikuli ya rais hapo jana, wakati viongozi wa serikali ya mpito rais Kiir na Makamu wake Machar walipokuwa na kikao na wanahabari Ikulu.

Gazeti la Sudan Tribune linaripoti kuwa imethibitishwa kuwa wanajeshi 150 kutoka pande zote mbili wameuawa katika makabiliano mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo tangu kuundwa kwa serikali ya mpito mwezi Aprili na kumalizika kwa machafuko.

Afisa mmoja wa kijeshi amenukuliwa akisema kuwa wanajeshi 35 wanaomtii Machar na 80 wanaomtii rais Kiir wameuawa huku kukiwa na hofu ya idadi hiyo kuongezeka.

Rais Kiir, na Machar wamesema hawafahamu ni kwanini wanajeshi hao waliamua kushambuliana.

Mashambulizi haya yalijiri siku moja baada ya wanajeshi wanaomuunga mkono Riek Machar kuwashambulia na kuwauawa wanajeshi watano wanaomuunga mkono rais Kiir katika kizuizi cha usalama jijini Juba.

Wakaazi wa Juba kwa sasa wanaishi kwa hofu baada ya mauaji haya, huku viongozi hao wakiwataka raia kuendelea kuwa watulivu kipindi hiki kigumu.

Mitaa ya jiji la Juba imebaki kimya bila ya watu kuendelea na shughuli zao za kawaida.