SUDAN KUSINI

Wanajeshi waendelea kupigana jijini Juba

Wanajeshi wa Sudan Kusini wakiwa wamejihami kwa bastola
Wanajeshi wa Sudan Kusini wakiwa wamejihami kwa bastola abc news

Mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali ya mpito wanaomuunga mkono rais Salva Kiir na wale wanaomuunga mkono Makamu wake wa kwanza wa rais Riek Machar yameshuhudiwa leo  jijini Juba, siku mbili baada ya mapigano kama haya kuzuka na kusababisha vifo vya wanajeshi 150.

Matangazo ya kibiashara

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaotoa misaada ya kibinadamu nchini humo wamethibitisha makabiliano hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Msemaji wa wanajeshi wanaomtii Machar Kanali William Gatjiath, ameliambia Shirika la Habari la Uingereza BBC kuwa Sudan Kusini imerejea tena vitani.

Aidha, amenukuliwa akisema rais Kiir anaonekana hana nia ya kutekeleza mkataba wa amani uliomaliza vita vya miaka miwili nchini humo, tuhma ambazo upande wa serikali haujajibu.

Ripoti kutoka Juba, zinasema  asubuhi ya leo hali ilikuwa mbaya na kusababisha safari za ndege za Shirika la Kenya kuahirisha safari zake kwenda Juba kwa sababu za kiusalama.

Wanajeshi wa Sudan Kusini
Wanajeshi wa Sudan Kusini channel4.com

Pia imeelezwa  mapigano hayo yalizuka Magharibi mwa jiji hilo eneo ambalo wanajeshi watifuu wa rais Kirr na wale wa Machar wanapiga kambi, huku wanajeshi wa Machar wakidai kushambuliwa katika ngome yao.

Mapigano haya mapya yamejiri pia siku moja tu baada ya nchi hiyo kuadhimisha miaka 5 ya uhuru wake bila ya shamrshamra zozote.

Ni mapigano mabaya sana kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu kurejea kwa Riek Machar nchini humo mwezi Aprili na kuungana na rais Kiir kuunda serikali ya pamoja baada ya miaka miwili ya vita.