UGANDA-KIZZA BESIGYE

Besigye aapa kuendelea kuipinga Serikali

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda FDC , Kizza Besigye, ameapa kuendelea na harakati zake za kuipinga Serikali ya Rais Yoweri Museveni, na kusema kwamba hakuna kitakachomrudisha nyuma katika kupigania haki za wananchi wa Uganda.

Kizza Besigye mbele ya vyombo vya habari, Kampala, Februari 13, 2016.
Kizza Besigye mbele ya vyombo vya habari, Kampala, Februari 13, 2016. Isaac Kasamani / AFP
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari, kwenye makao makuu ya chama hicho katika eneo la Najjanankumbi, jijini Kampala, Besigye, ambaye kwa zaidi ya miezi miwili alikuwa akizuiliwa kwenye gereza la Luzira akikabiliwa na kesi ya uhaini kabla ya kuachiwa kwa dhamana hapo jana, amessisitiza kuwa rais Museveni hakushinda uchaguzi wa mwezi Februari.

Aidha, amesema yeye pamoja na viongozi wengine waliojitoa kwa ajili ya kupigania haki, wataendelea kunyanyaswa na vyombo vya usalama na kwamba hilo halitakuwa kikwazo kwao.

Alipoulizwa kuhusu ni lini atakoma kuhamasisha maandamano na kuacha kuikosoa Serikali halali iliyochaguliwa Kidemokrasia, Besigye amesema wakati haujafika wa kufanya hivyo na ataendelea kupigania haki za wanyonge.