MALALA-SOMALIA

Malala: Ni hatari kuwarudisha wakimbizi wa Somalia nyumbani, hasa wasichana

Mshindi wa tuzo la Nobel na mwanaharakati wa masuala ya Elimu, Malala Yousafzai, akiwahutubia wakimbizi wa kambi ya Daadab, nchini Kenya, wakati akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa, 12 Julai, 2016.
Mshindi wa tuzo la Nobel na mwanaharakati wa masuala ya Elimu, Malala Yousafzai, akiwahutubia wakimbizi wa kambi ya Daadab, nchini Kenya, wakati akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa, 12 Julai, 2016. REUTERS/Thomas Mukoya

Wasichana wa Somalia wako hatarini kutoendelea kusoma na wana hatari ya kuishia kuolewa wakiwa wadogo, ikiwa watalazimishwa kuondoka kwenye kambi ya wakimbizi ya Daadab na kurudishwa nchini mwao, ambako vita dhidi ya Al-Shabab inaendelea, amesema mwanaharakati msichana raia wa Pakistan, Malala Yousafzai.

Matangazo ya kibiashara

Malala ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya elimu, aliyenusurika kuuawa kwenye shambulio la kundi la Taliban mwaka 2012, alisherekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 19 kwenye kambi ya wakimbizi ya Daadab, ambayo Kenya inataka kuifunga kwasababu za kiusalama.

"Tatizo ni kuwa hakuna shule za kutosha nchini Somalia," amesema Malala wakati akizungumza na shirika la habari la Ufaransa la AFP, huku akiwa ameketi kwenye moja ya madarasa ya shule zilizoko kwenye kambi hiyo.

Malala ameongeza kuwa "ikiwa wasichana hawa hawataenda shule, basi wataolewa wakiwa na umri mdogo, na hii ingekuwa sawa kama mimi mwenyewe ningeamua kurudi nchini mwangu, nisingeenda shule," alisema.

Kutoka kushoto, Malala Yousafzai, baba yake, na msichana, Rahma Hussein Noor wakizungumza na wanafunzi kwenye shule moja iliyoko kwenye kambi ya Daadab, nchini Kenya, Julai 12, 2016
Kutoka kushoto, Malala Yousafzai, baba yake, na msichana, Rahma Hussein Noor wakizungumza na wanafunzi kwenye shule moja iliyoko kwenye kambi ya Daadab, nchini Kenya, Julai 12, 2016 REUTERS/Thomas Mukoya

"Wewe ni kama mali ya mtu mwingine tu, na sikutaka hilo kamwe, nilitaka kuwa mwenyewe." alisema Malala.

Nchi ya Kenya, ambayo imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa Al-Shabab, inalenga kuwarudisha nyumbani zaidi ya raia laki moja na elfu 50 kutoka kambi ya Daadab ambayo ni makazi ya wakimbizi zaidi ya laki 3, wengi wakiwa ni raia kutoka Somalia.

Malala aliambatana na msichana mwingine raia wa Somalia mwenye umri wa miaka 19, Rahma Hussein Noor, ambaye alihamishwa kutoka Somalia yeye na familia yake mwezi October mwaka jana wakati baba yake alipojaribu kumuoza.

Maelfu ya wakimbizi wengi wakiwa watoto wa shule walikusanyika kwenye uwanja wa michezo kwenye kambi hiyo, kumsikiliza Malala Yousafzai, msichana mdogo zaidi duniani kuwa mshindi wa tuzo la Nobel.