BURUNDI-EALA-MAUAJI

Mbunge wa EALA auawa Burundi

Kwenye eneo la mauaji ya Hafsa Mossi, katika kata ya Mutanga, Mashariki mwa mji wa Bujumbura, Julai 13, 2016.
Kwenye eneo la mauaji ya Hafsa Mossi, katika kata ya Mutanga, Mashariki mwa mji wa Bujumbura, Julai 13, 2016. ONESPHORE NIBIGIRA / AFP

Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutoka Burundi, Hafsa Mossi ameuawa kwa kupigwa riasi Jumatano mapema mchana, wakati alikua akiondoka nyumbani kwake, kata ya Mutanga, wilayani Gihosha, mashariki mwa mji wa Bujumbura.

Matangazo ya kibiashara

Hafsa Mossi alikua mtu wa karibu wa Rais Pierre Nkurunziza.

Watu walioendesha mauaji hayo hawajajulikana, lakini wanasadikiwa kuwa walikua ndani ya gari ndogo aina ya Corolla TI yenye vio ambavyo si rahisi kumuona mtu aliyekua ndani.

Kabla ya kuwa Mbunge wa EALA, Hafsa Mossi aliwahi kushikilia nyadhifa muhimu katika utawala wa chama cha CNDD-FDD. Aliwahi kuwa msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari.

Kwenye akaunti yake ya Twitter, Rais Pierre Nkurunziza ameelezea kuhuzunishwa na mauaji ya Hafsa Mossi akisema kuwa Burundi na Jumuia nzima ya Afrika ya Mashariki wamepoteza mtu mwenye thamani.

"Mauaji ya Mhe. Hafsa Mossi ni kitendo kiovu na cha ujinga. Hii ni hasara kubwa kwa Burundi, familia yake na jumuiya yote ya Afrika Mashariki (EAC)."

Itafahamika kwamba Hafsa Mossi aliwahi kuwa Mwandishi wa habari, aliitumikia redio ya taifa RTNB miaka ya nyuma, kabla ya kujiunga na redio Channel O, kabla ya kubadilisha jina na kuwa shirika la utangazaji la SABC nchini Afrika Kusini, na mwishowe alifanya kazi katika shirika la utangazaji la BBC, katika Idhaa ya Kiswahili, kabla ya kurejea nyumbani miaka ya 2004 na kujiunga katika maisha ya kisiasa.

Hali ya usalama imeendelea kudoroa katika maeneo mbalimbali ya nchi ya Burundi, hasa mjini Bujumbura, ambapo mauaji ya kuvizia yamekithiri.