KENYA-BAN

Ban: Kama hatutaki wananchi waandamane, tutatue matatizo ya kiuchumi

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa biashara na maendeleo wa UNCTAD, 17 Julai, 2016
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa biashara na maendeleo wa UNCTAD, 17 Julai, 2016 UNCTAD handout

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema kuwa, migogoro na maandamano yanayoshuhudiwa hivi sasa kwenye mataifa mengi duniani, imetokana na hali mbaya ya uchumi pamoja na kukosekana kwa utashi wa kisiasa wa viongozi kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wao.

Matangazo ya kibiashara

Ban Ki Moon, amesema haya, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa kuhusu biashara na maendeleo linalofanyika jijini Nairobi nchini Kenya, chini ya shirika la umoja wa Mataifa, UNCTAD.

Ban amesema kuwa, utawala mbaya na kuendeleo kuporomoka kwa uchumi wa dunia, ndiko kunakosababisha wananchi kuchoka na kukosa uvumilivu dhidi ya Serikali zao, na hasa vijana ambao wameendelea kujiunga na makundi ya kijihadi kutokana na kukosa usaidizi.

Ban ki Moon amesema ni jukumu la kila kiongozi duniani kuhakikisha wanakabiliana na hali mbaya ya kiuchumi na kuhakikisha wanafikia malengo ya kuwa na dunia yenye maendeleo endelevu kama malengo ya umoja wa Mataifa yanayovyoelekeza ifikapo mwaka 2030.

Wataalamu wa masuala ya uchumi na biashara wanaona kuwa, hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya mazungumzo na makubaliano kadhaa yaliyowahi kufikiwa kuhusu kupiga vita umasikini na kuwaletea maendeleo wananchi.