KENYA

Kenya: Polisi wanaoshtumiwa kumuua Wakili Willie Kimani wafunguliwa mashtaka

Maafisa wa polisi wanaotuhumiwa kumuua wakili Willie Kimani wakiwa Mahakamani jijini Nairobi
Maafisa wa polisi wanaotuhumiwa kumuua wakili Willie Kimani wakiwa Mahakamani jijini Nairobi ibtimes

Mahakama Kuu  jijini Nairobi nchini Kenya imewafungulia mashtaka ya mauaji maafisa wanne wa polisi kwa tuhma za kuhusika na kifo cha wakili wa haki za binadamu Willie Kimani, mteja wake na dereva taxi wiki mbili zilizopita.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa mashtaka amewataja maafisa hao wa polisi kuwa
Fredrick Leliman, Leonard Maina Mwangi, Stephen Chebulet na Silvia Wanjiku Wanjohi.

Washukiwa hao walikamatwa baada ya kuhusishwa na mauaji hayo ambayo yalisababisha maandamano ya wiki moja ya mawakili katika miji mbalimbali nchini humo kulaani mauaji hayo.

Uchunguzi wa daktari wa serikali Johansen Oduor umebaini kuwa wakili huyo na wenzake wawili walipigwa na kitu kizito na baadaye kuyongwa tarehe 23 mwezi Juni.

Mwandishi wa RFI Kiswahili James Shimanyula ambaye amekuwa Mahakamani, amesema kulikuwa na watu wengi waliofika Mahakamani hasa mawakili, jamaa ndugu na marafiki wa marehemu hao.

Aidha, Shimanyula amesema kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 16 mwezi ujao na  washukiwa hao wataendelea kuzuiliwa rumande kusubiri kutajwa kwa kesi.

Upande wa mashtaka umesema mashahidi 45 watafika Mahakamani katika kesi hiyo.

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai umeahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha kuwa haki inatendeka katika kesi hiyo.