KENYA-UNCTAD

Kenya yasema mataifa ya Afrika yanahitaji ushirikiano kutoka UN, sio misaada

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akihotubia mkutano wa UNCTAD
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akihotubia mkutano wa UNCTAD samrack

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kushirikiana na serikali za bara Afrika, kufanikisha maendeleo mbalimbali endelevu.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika siku ya pili ya Mkutano wa 14 Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD) unaofanyika jijini Nairobi, rais Kenyatta amesisitiza umuhimu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuweka fedha zao katika  miradi kama ya maji, afya na kilimo.

Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa bara la Afrika linahitaji ushrikiano wala sio msaada wa mara kwa mara kama inavyoshuhudiwa sasa.

“Hatuhitaji msaada, tunachohitaji ni ushirikiano, acha hayo mashirika ya Umoja wa Mataifa yaje tufanye kazi pamoja na sisi tusione matatizo tuliyonayo kama changamoto bali tuyaangalie kama fursa,” alisema rais Kenyatta.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la dunia la Biashara WTO Robert Azevedo amesema mataifa yanayoendelea hasa ya Afrika, amesema maendeleo endelevu yatafikiwa tu kufikia mwaka 2030 ikiwa mataifa husika yataanza jitihada za ndani kufikia malengo hayo.

Maelfu ya wajumbe wakiwemo marais kadhaa wa dunia wanakutana katika mkutano huo uliofunguliwa hapo jana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kujadili maswala mbalimbali ya biashara duniani.

Mkutano huo utamalizika tarehe 22.