KENYA-DRC

Mwanamuziki Koffi Olomide afukuzwa Kenya

Koffi Olomide Mwanamuziki maarufu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amefukuzwa nchini Kenya, baada ya kukamatwa hapo jana kwa kumpiga teke mnenguaji wake wa kike katika uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Koffi Olomide
Koffi Olomide oeildafrique.com
Matangazo ya kibiashara

Mkanda wa Video uliosambaa katika mitandao ya kijamii pindi tu baada ya Koffi mwenye umri wa miaka 60, kumshambulia mwanadada huyo ulilaaniwa na wakenya kupitia mitandao ya kijamii hasa Twitter lakini pia wabunge.

Mwanamuziki huyo alikamatwa jana usiku na polisi baada ya kumaliza mahojiano maalum katika kituo kimoja cha Televisheni nchini humo na kuzuiwa katika kituo cha polisi katika uwanja wa ndege.

Hii sio mara ya kwanza kwa mwanamuziki huyo ambaye kwa sasa anafahamika kwa wimbo wake maarufu wa “Ekotite” kukabiliwa katika hali hii ya kuwashambulia watu wakiwemo wanahabari.

Kurudishwa nyumbani jijini Kinshasa kunamaanisha kuwa tamasha lake lililotarajiwa kufanyika leo Jumamosi jijini Nairobi halitafanyika tena.