KENYA

Visa vya uteketezwaji moto wa mabweni katika shule za Sekondari vyaongezeka Kenya

Wazazi, Walimu na maafisa wa Usalama wakikagua baadhi ya bweni liliteketezwa moto katika Shule moja ya Sekondari nchini Kenya
Wazazi, Walimu na maafisa wa Usalama wakikagua baadhi ya bweni liliteketezwa moto katika Shule moja ya Sekondari nchini Kenya West FM

Kenya imeendelea kushuhudia ongezeko la wanafunzi wa Shule za Sekondari kuteketeza moto mabweni yao kwa sababu mbalimbali katika siku za hivi karibuni, ikiwemo kunyimwa nafasi ya kuangalia michuano ya soka ya bara Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Tukio la hivi punde ni kuteketezwa moto kwa bweni la Shule ya wavulana ya Lang'ata jijini Nairobi na kusababisha majeraha ya wanafunzi 15 waliokuwa wanajaribu kuokoa mali zao.

Ongezeko la visa hivi, vimeendelea kuzua maswali mengi  kuhusu kiwango cha nidhamu kwa wanafunzi hao wa shule za sekondari huku Wizara ya elimu ikilaumiwa na baadhi ya wadau wa elimu kuchangia ongezeko hili.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Chumani katika Kaunti ya Kilifi Pwani ya nchi hiyo
Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Chumani katika Kaunti ya Kilifi Pwani ya nchi hiyo Baraka FM

Waziri wa Elimu Fred Matiangi amejitetea dhidi ya madai kuwa sera mpya alizoleta katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa masomo lakini na kupiga marufuku wazazi kuwatembelea watoto wao na maombi katika muhula wa tatu wakati wa kipindi cha mtihani wa kitaifa umechangia suala hili.

Aidha, ameongeza kuwa mabadiliko haya ni ya kuleta nidhamu na kuhakikisha kuwa mitihani inafanyika kwa njia nzuri ili kuzuia visa vya wizi wa mitihani kama ilivyoshudiwa katika siku zilizopita.

Pamoja na hilo, Walimu Wakuu wa Shule hizo wameshtumiwa kuchochea ongezeko la visa hivi kwa madai ya kupinga mabadiliko haya ya Waziri.

Mamia ya wanafunzi wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuhusika na uchomaji moto wa mabweni hayo huku wadau wengine wakitaka serikali kurejesha adhabu ya kupigwa viboko kwa wanafunzi wa Sekondari.